Pigeni kwenzi kinyago, mjiumize
vidole,
Geuzieni visogo, ili nisiende mbele,
Mnajipa tu mizigo, mambo yangu
palepale,
Acheni kujisumbua, sivurugwi
kirahisi.
Mnatunisha misuli, kunitishia
mwenzenu,
Mwanishuparia kweli, hamjali ndugu
yenu,
Mnaninyang`anya mali, mnataka ziwe
zenu,
Mnakazana kwa nguvu, mpate
kunivuruga.
Mkiniona mnyonge, si kwamba
nimedhoofu,
Natulia nijipange, nisijedondoka bufu!
Sio nacheza madange, mnione
mpumbafu,
Sivurugwi kirahisi, maana niko
ngangali.
Sawa maisha magumu, watu
tunajikokota,
Sithubutu kunywa sumu, roho yangu
ikakata,
Kwani Mungu mkarimu, nikiomba
nitapata,
Maadui sawa wapo, hata hivyo
sivurugwi.
Ahsante adui zangu, mnanipa ujasiri,
Hongera rafiki zangu, mwanifanya
mashuhuri,
Mnaponipiga rungu, nazidi kuwa
mahiri,
Sivurugwi kirahisi, ipo kazi
kunizima.
Chura akipigwa teke, afurahi
kwelikweli,
Maana ni faida kwake, inapungua
safari,
Nikipigwa nivunjike, ndio naota
misuli,
Sivurugwi kirahisi, acheni
kujisumbua.
Haya maisha ya sasa, ni magumu kwelikweli,
Kama mtu huna pesa, yatakupiga
kabali,
Tena yatakutikisa, uchungulie
kabuli,
Ndo mana siwi mvivu, nisije
nikavurugwa.
Kwanza watu wana wivu, wanaweza
kukuua,
Wale walo na mabavu, waweza
kukusumbua,
Dunia tambala bovu, acha
kutuongopea,
Watu ndo walowabovu, wanavurugana
ovyo.
No comments:
Post a Comment