Tuesday 26 April 2016

KILIMO CHA ZAO LA TIKITI MAJI ‘KILIVYOWATOA’ VIJANA KILOMBERO

KILIMO CHA ZAO LA TIKITI MAJI  ‘KILIVYOWATOA’ VIJANA

Na  Mhariri wa Blog






Suala  la ajira limekuwa kilio cha mda mrefu miongoni mwa Watanzania wengi hususani vijana, ambao ni nguvu kazi ya Taifa.
 Vijana wamekuwa wahanga wakubwa wa kukosa ajira na fursa kujikwamua kiuchumi. Hali ambayo inasababisha kundi  kubwa la vijana kuyahama makazi yao na kwenda mijini kwa kile wanachokiita, `` kutafuta maisha”  wakidhani kwamba  mjini ndiko sehemu pekee ambako ni rahisi kupata ajira, la hasha, maisha ya mjini yamekuwa tofauti sana na yale ambayo vijana wengi wamekuwa wakiyafikiria na hatimaye wengi huishia kutangatanga tu pasipo mafanikio.
Kuna fursa nyingi sana ambazo zikitiliwa mkazo,zinaweza kutoa ajira, watu waishio bonde la Kilombero, Mkoani Morogoro wamepata Baraka kubwa ya kuwa na eneo nzuri la shughuli za kilimo, mbali na shughuli za kilimo cha mpunga na mahindi ambazo hufanywa na wakazi wa Kilombero, pia bonde hilo limeonekana kuwa na rutuba iliyosafi sana kustawisha zao la matikiti maji.
Zao hilo linapendwa na watu wengi sana  mkoani Morogoro na sehemu zingine nchini, tokana na mahitaji yake katika mwili, kwa mfano, Tikiti maji mbali na kuwa na radha nzuri pia ni chanzo kizuri cha vitamini. Katika tunda hilo kuna Vitamin A, inayosaidia kuboresha afya ya macho na pia kuondosha sumu mwilini; Vitamin C, inayosaidia kuboresha kinga, kuponya majeraha, kukinga uharifu wa seli, kuboresha afya meno na fizi; na vitamini B6, inayosaidia ubongo kufanya kazi na pia kuibadilisha protini kuwa nishati.
Tunda la tikiti maji lina kiwango kikubwa cha lycopene kuliko tunda lolote au mboga za majani.
Ikiwa familia yako inaishi kwenye eneo lisilo na vyanzo vya madini ya potasiam, unaweza kuwapa tikiti badala yake. Lina uwezo mkubwa wa kusaidia misuli na mfumo wa fahamu kwa ujumla kufanya kazi zake vizuri.
Tikiti pia lina amino asidi na virutubisho vingine vinavyosaidia kurahisisha mtiririko wa damu kwenye mishipa yake.
Kuna faida nyingi sana ambazo wataalamu wanazidi kuzielezea kutoka katika tunda hilo, hivyo  kusababisha zao hilo kuongezeka kwa soko lake. Kwahiyo hiyo ni fursa tosha sana kwa vijana wa Jimbo la kilombero kujiajiri.
Zao la tikiti lina hitaji jua la kutosha, maji mengi, na ardhi yenye rutuba na hivyo vyote vinapatikana katika bonde hilo, tena zao hili linaweza kulimwa hata mara nne kwa mwaka inategemeana na mbegu, pia endapo ukame utazidi pia unaweza kulima kwa kumwagilia ambapo kila shina linahitaji lita kumi za maji, ambazo utamwagalia asubuhi na jioni, laikini bonde la kilombero limebarikiwa kuwa na chemchem nyingi sana za maji ambazo zimetoka kwenye mto kilombero unaotenganisha wilaya ya Ulanga na kilombero hivyo zoezi la umwagiliaji sio changamoto sana.
Ngoja niwape mfano namna kijana anavyoweza kufaidika kutokana na zao hili la tikiti, matikiti maji hukua haraka kama mimea mingine itambaayo  ya jamii yake kama vile maboga, matango na maskwash. Zao hili litaonekana gumu kidogo kama ni mara ya kwanza kuanza kwasababu linahitaji umakini kiasi, ila pia ni zao jepesi sana kulimudu endapo utazingatia taratibu zake za kilimo na pia litakuwa zao kombozi kwa vijana wenye nia ya kujikwamua kimaisha, udongo wa bonde la kilombero lina rutuba nzuri na lina udongo unaotuhamisha maji,hivyo linatumia mbolea kidogo sana kutoka viwandani, ili kuweza kupata mavuno makubwa kutoka zao hili unaweza kuongeza kutumia mbolea kidogo za samadi, na za viwandani zenye naitrojen na potasiam ili kuimarisha zaidi mazao yako.
Zao la tikiti linaanza kukomaa kuanzia siku ya 80-120 kulingana na aina ya mbegu, zingine huanzia kuvunwa siku ya 54-60.
 Kwa mfano ukipanda mbegu aina ya ``sugar baby”  unaweza kuvuna baada ya siku 60 tangu siku ya 3-5 za kukaa ardhini, kwahiyo kwa mwaka unawezsa kulima hata mara 4. Na ukipanda kwa nafasi ya mita 2 kwa 2 na kila shimo ukiweka mbegu mbili ambazo zinatoa wastani wa matunda matano.
Hivyo kwa nafasi hiyo kwa ekari moja endapo ukaweza  kupanda mashimo 200-240, kwa makadilio ya chini.
Idadi ya matunda: Mashimo x Matunda kwa shimo x ekari ( 200x5x1=1000 )
Mapato:  Wastani wa shilingi 1000 kwa tikiti  x idadi ya tikiti kwa eneo la ekari 1, ( 1000 x 1000 = 1,000,000 ) hiyo ni kilimo cha mara  moja tu, je, ukilima mara mbili na zaidi utakuwa wapi?


Huo ndio uhalisia wa zao hilo na kama kijana ukaitumia vizuri fursa hii ni lazima ufikie malengo uliyo jiwekea, na zaidi sana kama utaendana na kasi ya sera ya HAPA KAZI TU, na kweli ukawa unajituma katika kazi, basi kuna uwezekano mkubwa sana wa kufanya mabadiliko juu ya maisha yako badala ya kukaa vijiweni na kulalamikia selikari haitoi ajira kwa vijana.

No comments: