Na Fatma Salum (MAELEZO).
Serikali kupitia Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) imesema hivi karibuni itaanza msako mkali wa kuwatafuta na kuwakamata wauzaji wa dawa zinazokatazwa pamoja na vipodozi vikali ambao wanajitangaza kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii.
Hayo
yamesemwa na Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Umma kutoka TFDA Bi.
Gaudensia Simwanza wakati wa mahojiano na mwandishi wa habari hii kuhusu
kuibuka kwa watu wanaotangaza biashara ya dawa na vipodozi ambavyo
Serikali imevipiga marufuku.
Akitaja
bidhaa hizo Bi. Simwanza alisema ni pamoja na dawa za kuongeza ukubwa
wa viungo vya mwili, kupunguza uzito wa mwili na vipodozi vyenye
kemikali za kuchubua ngozi bidhaa ambazo zinasababisha madhara makubwa
kwa binadamu ikiwemo ugonjwa wa Saratani.
“Kumezuka
wafanyabiashara holela wanaotumia mitandao ya kijamii kama vile
Instagram, Facebook, Whatsup Groups na kwengineko kutangaza biashara ya
dawa na vipodozi vyenye kemikali hatari ambavyo vimepigwa marufuku na
TFDA hivyo wanaohusika wajiandae, hivi karibuni tutaanza
kuwashughulikia.” Alisema Simwanza.
Alieleza
kuwa TFDA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi wameandaa mkakati
madhubuti wa kuhakikisha wanawabaini na kuwakamata wafanyabiashara wote
wanaouza dawa na vipodozi hivyo kupitia mitandao na kuwachukulia hatua
ikiwemo kuwafikisha mahakamani au kuwatoza faini.
“Wengi
wa wafanyabiashara hao hawaweki anuani za maeneo wanayopatikana na
hawana maduka rasmi bali huweka namba za simu za mkononi lakini kwa
kutumia vyombo vya dola tutawabaini tu na kuwatia mbaroni.” Alisisitiza
Simwanza.
Kwa
upande wake Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
(TCRA) Bw. Innocent Mungy amewatahadharisha watumiaji wa huduma za
mawasiliano hasa matangazo ya biashara kuwa makini na matangazo hayo
kwani baadhi ya wafanyabiashara hizo wanaweza kuwa ni watu wenye nia
mbaya.
Hivi
karibuni kumeibuka wimbi la wafanyabiashara wa dawa mbalimbali pamoja
na vipodozi ambao wanajitangaza kupitia mitandao ya kijamii na kuna
baadhi ya watu wananunua bidhaa hizo bila ya kuhakikisha usalama wake
jambo ambalo ni hatari kwa afya zao.
No comments:
Post a Comment