Sunday, 29 May 2016

WADAU WA ELIMU WAHIMIZWA KUCHANGIA TATIZO LA UPUNGUFU WA MADAWATI



Wilaya ya Kilombero kupitia Halmashauri zake za wilaya ya Kilombero na Halmashauri ya Mji Ifakara inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa madawati (25,021) elfu ishirini na tano na ishirini na moja.
Mkuu wa wilaya ya Kilombero Mh Lephy Gembe ameyasema hayo katika kikao cha pamoja na wadau mbalimbali wa Elimu aliowakaribisha katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Kilombero ili kujadiliana nao  pamoja na kuwapa taarifa za changamoto ya upungufu wa madawati kwa shule za msingi wilayani Kilombero kupitia taarifa yake iliyowasilishwa na Afisa Elimu Msingi Ndugu Yona Mzimya.
Wananchi wa wilaya ya Kilombero wameitikia kwa kasi kubwa fursa ya Elimu bila malipo hali iliyoleta ongezeko kubwa la wanafunzi walioandikishwa kwa mwaka wa masomo 2016, awali jumla ya wanafunzi 11,088  walitarajiwa kuandikishwa darasa la kwanza huku idadi halisi ya walioandikishwa kuanza elimu ya darasa la kwanza ikifikia wanafunzi 16,111 ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 5,023 zaidi ya makisio ya awali.
Asilimia sitini na mbili (62 %) ya wanafunzi wote wa shule za msingi waliopo katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara wanakaa chini huku idadi  yao ikiwa ni wanafunzi 15,990 kati ya wanafunzi 25,722 ambayo ni idadi ya wanafunzi wote wa shule za msingi ndani ya Halmashauri ya mji wa Ifakara.
Kwa upande wa Halmashauri ya wilaya ya Kilombero jumla ya wanafunzi 43,567 wanakaa chini ikiwa ni sawa na asilimia Hamsini na nane nukta nane tano (58.85 %) kati ya wanafunzi 74,037 ya wanafunzi wote waliopo katika shule za msingi zilizopo katika Halmashauri ya wilaya Kilombero.
Jumla ya Gharama ya shilingi bilioni moja milioni miambili  hamsini na moja na elfu hamsini (1,251,050,000/=) zinahitajika ili kutengeneza madawati 25,021 kwa gharama ya shilingi elfu hamsini (50,000/=) kwa kila dawati moja, Mchanganuo wa gharama ya shilingi elfu hamsini kwa kila dawati ni gharama za ufundi, gharama za misumari, na gharama za usafirishaji wa madawati katika maeneo husika mara baada ya madawati kukamilika.
Wilaya imejiwekea utaratibu wa kupata mbao zitakazotumika kutengenezea madawati hayo kwa kuvuna misitu iliyopo katika ngazi ya kata kupitia vijiji vyake katika kila eneo kwa kufuata utaratibu wa kisheria kwa kushirikiana na wakala wa misitu na idara ya maliasili ili kutumia fursa za mali asili zilizopo kukabiliana na changamoto ya madawati ndani ya wilaya ya Kilombero hususani katika ngazi ya kata na vijiji.
Katika kikao hicho Jumla ya shilingi milioni sita na elfu sabini na tano ziliahidiwa na wadau ikiwa ni sehemu ya michango yao ili kukabiliana na changamoto ya madawati kwa shule za msingi ambapo pesa taslim iliyopatikana ni shilingi elfu ishirini na tano huku wadau hao wakijiwekea malengo ya kuwasilisha ahadi zao mpaka kufikia tarehe 30/05/2016.


No comments: