Mgombea urais wa
chama cha Democratic nchini Marekani Hillary Clinton amejitangaza
mshindi kwenye mchujo wa chama hicho katika jimbo la Kentucky.
Huku
kura nyingi zikiwa zimehesabiwa katika jimbo hilo, na uongozi wake
ukiwa chini ya 0.5%, Bi Clinton ametangazwa kuwa mshindi asiye rasmi na
mmoja wa maafisa katika jimbo hilo.
Katika jimbo jingine la Oregon, ambalo pia lilifanya mchujo Jumanne, Seneta Bernie Sanders ameibuka mshindi.
Bi Clinton, ambaye anaongoza kwa wajumbe katika chama cha Democratic, ana matumaini makubwa ya kupata uteuzi Julai.
Alison
Lundergan Grimes, mwenyekiti wa bodi ya uchaguzi ya Kentucky, ameambia
CNN kwamba matokeo yasiyo rasmi yanaonesha Clinton atapata ushindi
mwembamba katika mchujo Kentucky.
Muda mfupi baadaye, Bi Clinton
ameandika kwenye Twitter: "Tumeshinda Kentucky! Nawashukuru sana nyote
mliojitokeza. Tuna nguvu zaidi daima tukiwa na umoja.”
Bw Sanders, akihutubia mkutano California Jumanne, alisema bado ataendelea na kampeni yake.
Katika
chama cha Republican, Donald Trump ameshinda mchujo, jambo ambalo si la
kushangaza kwani ndiye pekee aliyesalia kwenye kinyang’anyiro.
Chanzo BBC
No comments:
Post a Comment