MWANAMKE
USIPOTHAMINI MTOTO, HAKUNA ATAKEYEMTHAMINI.
Na,
Fulgence Makayula
0655887798
Mwanamke ni mama wa familia, na kiimani amebeba uponyoji wa mwanaume kwa kuwa ametokana na ubavu wa mwanaume. Hivyo mwanaume amebeba vidonda kwa ajili ya mwanamke na kwa sababu hiyo basi wawili huishi pamoja kwa kushirikiana katika kutekeleza majukumu mbalimbali.
Ukiachilia mbali nafasi mbalimbali ambazo baadhi
ya waandishi wa kazi za kifasihi kumwandika na kumchora mwanamke katika
mitazamo hasi, lakini bado mwanamke atabaki kuwa, ni jasiri kwani naamini
kuwa kama ingekuwa mimba ina zamu ya kulea na kuibeba, sina shaka kuwa wanaume
wengi wasingekubali kukaa nayo hata kwa siku moja. Na hivyo ingemlazimu mama
kuibeba tena mpaka atakapojifungua. Na hapo kidogo ndipo mwanamme angejifunza
thamani ya kubeba mimba na kuilea kwa muda wote wa miezi tisa mpaka kuijifungua
na kuendeleza malezi ya mtoto wake.
Pia, ni mchapakazi, mchumi, mwalimu yaani
waswahili wanasema katika kila sekta yuko vizuri. Na kama hauamini angalia
wanawake wengi wakienda kufanya manunuzi sokoni, wanavyopiga bajeti ili pesa
aliyopewa hata kama ni kidogo itoshe kununua mahitaji na ikiwezekana ibaki
walau salio kidogo la kuanzia kesho au akanunue vocha.
Huyu ndiye mwanamke ambaye baadhi ya wanaume
umdharau bila kugeuka nyuma na kuangalia upande wa pili wa sarafu, kwa haya
anapaswa pongezi kubwa kwani si jambo la kawaida kwa shughuli anazozifanya.
Ukienda kijijini utamkuta mwanamke kabeba mtoto
mgongoni, ndoo ya maji kichwani, bado kuni juu ya ndoo ya maji, jembe mkononi
na mengine kibao. Huku mme wake akitembea tena kwa ujasiri kabisa na jembe lake
moja bila hata wasiwasi wowote. Na mara tu wafikapo nyumbani bado mwanamke huyu
huyu anashughulika na kuwasha moto wa kuni au mkaa ili aandae chakula cha
familia huku baba akiwa amestarehe kabisa. Na pengine akimfokea mwanamama huyu
kwa nini chakula hakiivi haraka.
Lakini pamoja na kuwa na sifa zote hizo baadhi
yao siku hizi wamegeuka na kuwa zaidi ya simba au chui kwa vitendo ambavyo
vimekuwa vikilipotiwa na vyombo vya habari na matukio mengine kusambazwa kwenye
mitandao ya kijamii.
Siku hizi imekuwa ni kawaida sana kusikia mtoto
kawekwa kwenye jokofu na wengine kubanikwa kwenye “oven” na baadhi ya wadada wa
kazi, mara utasikia mtoto kachomwa na pasi ya umeme eti kisa kaiba shilingi mia
tano. Hii inasikitisha sana kwa watu ambao jamii inawaamini lakini kwa sasa
imani imeanza kupungua kwa wadada hawa wa kazi.
Ukiachilia mbali wadada wa kazi wapo baadhi ya
wakina mama ambao naweza kusema hawaujui uchungu na pia naweza kusema kwao
watoto ni kama waliwaokota tu na hawakuingia kwenye chumba cha kujifungulia
maarufu kama leba. Kwani karibu kila mwezi utasikia mtoto katupwa mtaroni au
karibu na jaa la taka. Na hapa ndipo najawa na wasiwasi kama huyu mtu
aliyefanya kitendo hiki ana akili timamu au kidogo waswahili usema zimempita
kushoto.
Hii inasikitisha sana na huleta hisia kali
mkiongoni mwa wanajamii na baadhi ya mashirika ya kutetea haki za kibinadamu na
watoto kuhusu ukatili huu wanaofanyiwa. Labda kidogo niwakumbushe video
ambayo ilikuwa maarufu sana mwishoni mwa mwaka 2014, ambayo ilikuwa
ikimwonyesha mfanyakazi wa ndani huko nchini Uganda alivyokuwa akimpiga
mtoto ambacho kwangu naweza sema ni kipigo kitakatifu. Ilikuwa ni video ya
kusikitisha na baada ya maamuzi ya mahakama ya kumfunga miaka mitatu jela
lakini bado wanaharakati wa haki xza watoto bado hawajaridhika na adhabu hiyo.
Na hapo ndipo usemi usemao uchungu wa mwana
haujuaye mama lakini cha ajabu baadhi ya mama hawaujui kiukweli uchungu
na thamani ya mtoto au watoto wao. Chonde chonde dada zangu mtatia aibu
na heshima na thamani yenu inashuka kwani hakuna mwanaume yeyote anayependa
kuwa na mwanamke katili, kwani wengi wao wafanyao vitendo hivi ni wale hata
bado kwenye ndoa hawajaingia.
Namalizia kwa msemo mmoja wa Kiswahili usemao “
Usipoziba Ufa utajenga ukuta” na “ Mchelea mwana hulia mwenyewe” kwa maana
uchungu wa mwana aujuaye mama hivyo Napata ujasiri wa kusema kama mama
asipothamini uchungu wake kwa mwanaye hakuna atakaye weza kuthamini na kamwe
baba hatojali mtoto kama mama ukishindwa kumtunza mwanao.
No comments:
Post a Comment