Friday, 18 March 2016

MKWASI SIAFU

Image result for siafu



Ndiye mimi ni mkwasi, muenda pole wa mwendo,
Siwanyang'anyi nafasi, mi kiota cha upendo,
Ni kiwiji mla nyasi, sitaharaki kwa tendo,
Siafu wakiungana, nyoka atakasirika


Nimezipata tetesi, sizifanyii mshindo,
Mwanipalia manyasi, kunipigilia nyundo,
Mchora makaratasi,hachori chake kifundo,
Siafu wakiungana,  nyoka atakasirika


Mfano mpanda ngazi, hurudia pale pale,
Msiniibie pumzi, nikateseka milele,
Kurudi nyuma si Kazi, wa nyuma huenda mbele,
Siafu wakiungana, nyoka atakasirika


Kovu mtu ulishika, wala hashiki madonda,
Haya mnayo nitwika,  ni mazito kuyashinda,
Kovu mtu ulishika,bila machungu kupanda,
Siafu wakiungana, nyoka atakasirika


Mengine si ya hakika, mnatakiwa kupima,
Kupima na kuandika, yenye mana na heshima,
Mikono tukijishika, na twende tukichechema,
Siafu wakiungana, nyoka atakasirika


Kauli ni tamu sana, ikipambwa jukwaani,
Kwa masifu ya Osana, yaimbwa kwa ushindani,
Kauli zinakingana,  zikitua sikioni,
Siafu wakiungana, nyoka atakasirika


Kaumbo kangu kembamba, vazi langu la makama,
Nina akili ya samba, ruhusa yangu kusema,
Wananilisha kitimba, ili wapate rehema,
Siafu wakiungana, nyoka atakasirika


Vyakula vingi vitamu, nakura nikipendacho,
Vingine tena hadimu,  nachagua kiwa macho,
Na vingine vya msimu, huunda vipochopocho,
Siafu wakiungana, nyoka atakasirika


Miruzi mingi nyikani, mbwa huenda mrama,
Mpishi pika jikoni, chakula kiwe salama,
Staharaki starani, msije nipa kilema,
Siafu wakiungana, nyoka atakasirika


Na kura chakura changu, tamanio langu moyo,
Nayaepuka machungu, kula chukio la moyo,
Simsawishi mwenzangu, wa Moro na bagamoyo,
Siafu wakiungana, nyoka atakasirika


Chagueni mpendacho,  kuyashibisha matumbo,
Kuleni mkiwa macho,  msishikiwe kwa fimbo,
Mkala wakitakacho, mkipumbazwa kwa nyimbo,
Siafu wakiungana, nyoka atakasirika



No comments: