Mjadala umeshika kasi mitaani, mitandaoni na kila mahali baada ya Mahakama ya wilaya ya Kilombero kumhukumu kutumikia kifungo cha miezi sita jela bila faini Mbunge Wa jimbo la Kilombero Mhe. Peter Lijualikali (30) kwa kosa la kufanya fujo na kusababisha taharuki katika maeneo ya ukumbi Wa halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.
Mbunge huyo, akiwa mshtakiwa namba moja pamoja na mwenzie Stephano Mgata (35) walitenda kosa hilo Machi 1, 2016 saa 4 asubuhi Kwenye kikao cha Baraza la Madiwani katika eneo la Kibaoni ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro.
Imeelezwa kuwa kwa pamoja walifanya fujo kinyume na kifungu namba 89 kifungu kidogo cha kwanza B, cha kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002, ambapo washtakiwa walikana mashtaka na hivyo kufanya kesi kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili na upande wa mashtaka ukathibitisha bila kuacha shaka.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Kailima Ramadhan ameibuka na kukata kiu ya wananchi ya kutaka kujua endapo baada ya hukumu hiyo Mhe. Lijualikali ataendelea kuwa mbunge.
Akihojiwa na TBC One wakati wa taarifa ya habari ya saa mbili jana usiku, Bw. Kailima aliweka bayana kwamba mbunge huyo ataendelea na wadhifa wake kwa kuwa sheria inasema ili kupoteza kiti ni lazima uwe umepewa adhabu ya kifungo cha ZAIDI ya miezi sita jela.
"Ibara ya 67(2)(c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaeleza mambo yanayotoa sifa ya kuwa Mbunge kutoka madarakani ni kifungo cha zaidi ya miezi sita jela. Huyu bwana kafungwa miezi sita kwa hiyo bado hajapoteza sifa za kuendelea kuwa mbunge akiwa gerezani na baada ya kumaliza kifungo chake", alisema Bw. Kailima.
No comments:
Post a Comment