Saturday 5 November 2016

MAKALA: MIGOGORO YA ARDHI YAPUNGUA NCHINI KATIKA KIPINDI CHA MWAKA MMOJA WA SERIKALI YA JPM

May Simba na Lorietha Lawrence-MAELEZO

Ardhi ni kiwanda mama kwa maisha ya Watanzania na pia ni kichocheo kikuu cha ukuaji wa sekta mbalimbali za uchumi nchini.

Maendeleo ya sekta ya ardhi nchini yamekabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo migogoro ya muda mrefu baina ya jamii na wawekezaji, umiliki usio rasmi pamoja na ujenzi wa makazi holela.

Kuongezeka kwa migogoro ya matumizi ya Ardhi nchini kumesababisha Serikali kuboresha Sera ya Ardhi ya mwaka 1995.

Katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Tano, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imejitahidi kwa kiasi kikubwa kupunguza migogoro ya ardhi iliyokuwa kero kwa wananchi walio wengi.
 
Taarifa ya Wizara hiyo inasema jumla ya migogoro 1,378 iliripotiwa Serikalini hadi kufikia Oktoba 2016, ambapo migogoro 690 ilitatuliwa kiutawala.
 
Aidha jumla ya mashauri 3,968 yalitolewa maamuzi katika Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya.
 
Wizara hiyo pia imefanikiwa kumaliza mgogoro wa muda mrefu uliodumu kwa Zaidi ya miaka 15 katika maeneo ya Chasimba iliyopo katika eneo la Wazo Hill Jijini Dar es Salaam ambapo zaidi ya hekari 200 ya ardhi zilizokuwa na mgogoro baina ya wananchi na Uongozi wa kiwanda cha saruji cha Twiga umetatuliwa.

Migogoro mingine iliyotatuliwa kwa kipindi  hicho ni pamoja na ule wa shamba la Kapunga  Wilaya ya Mbarali, Mkoani Mbeya baina ya wananchi wa Kapunga na mwekezaji wa Kapunga Rice Project Limited mgogoro huuuliodumu kwa miaka 10, ambapo hekta 1,780 zimerejeshwa kwa wananchi.
 
Katika upande wa uboreshaji wa huduma kwa umma, Wizara imeimarisha utendaji kazi katika kituo cha huduma kwa wateja kwa kuongeza idadi ya watumishi, vifaa na aina ya huduma za ardhi zinazotolewa. 

Kutokana na maboresho hayo, idadi ya siku za kuandaa hati imepungua kutoka zaidi ya siku tisini (90) hadi kufikia chini ya siku sitini (60).

Aidha Wizara ndani ya kipindi cha mwaka mmoja, imeunda Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya mapya 47.

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kipentekosti na Mwenyekiti wa  Kamati ya Maadili, Amani, na Haki za Binadamu,  Askofu William Mwamalanga alipongeza mafanikio yaliyopo sasa katika  sekta ya ardhi, hatua inayotokana na Uongozi imara wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli.

Askofu Mwamalanga anasema utafiti uliofanywa na kamati yake umebaini kuwa asilimia 91 ya migogoro ya ardhi hapa nchini imepungua.

“Kamati ilifanya tafiti katika ngazi za Mikoa , Wilaya na Kata zote na kubaini kuwa migogoro ya ardhi nchini imepungua sana ukilinganisha na hali ilivyokuwa  hapo awali”, alisema Askofu Mwamalanga.

Askofu Mwamalanga  aliongeza kuwa mbali na kutatuliwa kwa migogoro ya ardhi pia  wafanyakazi  wa Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi  wamekuwa wakifanya kazi kwa  maadili na uadilifu mkubwa.  

Aliongeza kuwa katika kipindi cha nyuma sekta ya ardhi ilikuwa ikiongozwa kwa rushwa lakini katika uongozi wa Rais,Dkt.Magufuli kumekuwepo na hofu ya rushwa na uwajibikaji huku kila mtu akiwa mlinzi wa mwenzake.

Kwa mujibu wa Askofu Mwamalanga utafiti huo pia umebaini kuwa wafanyakazi wa sekta ya Ardhi katika halmashauri wamekuwa wakitoa ushirikiano wa hali ya juu katika kuhakikisha migogoro inatatuliwa kwa muda na wakati uliopangwa.

No comments: