Wakati leo ni mwaka mmoja tangu matokeo ya Uchaguzi Mkuu Zanzibar yafutwe Oktoba 28, 2015, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amemtuhumu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kuwa ndiye aliikwamisha nchi kwa kupindua maamuzi ya wananchi.
Maalim Seif alisema kutokana na uamuzi huo, ndiyo maana mpaka sasa mwenyekiti huyo ameshindwa kuibuka hadharani akielewa alibeba dhima ya Wazanzibari na Watanzania wote wapenda amani.
Maalim Seif aliyasema hayo jana alipofanya ziara ya siku moja katika wilaya zote saba za Unguja katika kumbukumbu ya mwaka mmoja, tangu Jecha alipofuta uchaguzi huo.
Maalim Seif aliita siku hii ‘black October’ akisema ndiyo siku Jecha alitekeleza kwa makusudi kufuta ndoto ya Wazanzibari ya kupata viongozi wanaowataka.
“Jecha ndiye aliyesitisha ndoto yetu ya kuwa Singapore, alipindua demokrasia na kufuta matokeo bila ya kuwapo kifungu chochote cha Katiba kinachotoa mamlaka hiyo,” alisema Maalim Seif.
Makamu huyo wa kwanza wa Rais mstaafu, alisema kuwa kabla ya Jecha hajatekeleza azma hiyo ovu, waangalizi wote wa uchaguzi kutoka ndani na nje ya nchi na ZEC wenyewe walijiridhisha na kutoa tamko kuwa uchaguzi ulikuwa huru na wa haki.
Waangalizi hao ni pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Madola, Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Bara la Afrika (SADC), Umoja wa Ulaya (EU) na Umoja wa Afrika (AU).
“Nasema alichotekeleza Jecha ni dhuluma na mapinduzi ambayo yalilenga kupindua maamuzi halali ya wananchi wa Zanzibar,” alisisitiza Maalim Seif akiwahutubia viongozi na watendaji wa CUF wa wilaya za Unguja.
Alisema yeye na viongozi wenzake wamekuwa wakiwatuliza wananchi na kwenda nao bega kwa bega, wakielewa hakuna popote umma ulipodai haki yao duniani kwa njia za kistaarabu na za kidemokrasia wakashindwa.
“Hivyo tambueni kuwa kimya kingi kina mshindo na haki yetu iliyoporwa haipo mbali kuipata kwani baada ya dhiki ni faraja,” alisema Maalim Seif.
“Jueni kuwa katika kutekeleza hayo zipo njama za waziwazi za kutaka kuipitisha Katiba ambayo haikupendekezwa na Watanzania kupitia maoni yaliwasilishwa kwa Tume ya Jaji Joseph Warioba,” alisema Maalim Seif.
Maalim Seif alisema miongoni mwa njama hizo ni mazungumzo yanayoendelea sasa kujaribu kuibua utaratibu wa kura ya maoni ili kuipitisha Katiba hiyo, chini ya usimamizi wa ZEC na NEC.
Alisema miongoni mwa njama za kuififisha Zanzibar ni mpango wa utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi na kuwakosesha wananchi fursa ya kufaidi raslimali zao.
Jecha hakupatikana jana kuzungunzia madai hayo, lakini Naibu katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai alipoulizwa alisema kwa sasa wapo katika mkakati wa kuimarisha chama katika ngazi zote yakiwamo matawi yao.
“Unajua sisi hatuzungumzii tena hayo, uchaguzi ulikwishafanyika na Serikali ikaundwa na sasa inafanya kazi, la msingi tunaimarisha chetu,”alisema Vuai aliyeko katika ziara ya kichama kisiwani Pemba.
Akizungumza katika ofisi za CUF Wilaya ya Kati Unguja, Maalim Seif alisema, “Nataka nikwambieni kilichotendeka kupitia Baraza la Wawakilishi la Zanzibar hivi karibuni wakidai kujadili sheria ya uchimbaji mafuta, ni kiini macho tu, maana hatujaona mabadiliko yoyote katika Katiba ya Jamhuri tukielewa kwamba jambo hilo bado ni suala la Muungano.”
Maalim Seif alihoji pia uhalali wa tamko la SMZ wa kumzuia asiongee na wananchi misikitini, akisema hiyo ni katika njama za kumnyamazisha asiyaeleze hayo.
Hivi karibuni, Waziri wa Nchi, Ofisi za Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohamed Aboud Mohamed alipiga marufuku hatua ya Maalim Seif kutembelea na kuongea na wananchi misikitini.
Kufuatia hatua hiyo Maalim Seif alihoji akisema, “Je, Mohamed Aboud haelewi wajibu wake, mbona hatujamsikia akikemea uvunjwaji wa Katiba na pia ukiukwaji wa Sheria Na. 5 ya Vyama Vingi vya Siasa ya Mwaka 1992, inayotoa ruhusa kufanya mikutano na maandamano, hayaoni hayo, hajui kuwa yamepigwa marufuku kinyume na Katiba?”
No comments:
Post a Comment