Fujo zimezuka katika mji mkuu wa Gabon, Libreville baada ya Rais Ali Bongo kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais uliofanyika Jumamosi.
Mgombea wa upinzani Jean Ping amesema watu wawili wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa baada ya vikosi vya usalama kuvamia makao makuu ya chama chake.
Serikali imesema inawaandama "wahalifu wenye silaha" ambao awali walikuwa wameteketeza majengo ya bunge.
Bw Ping amepinga matokeo ya urais ambayo yalionyesha Rais Bongo alishinda uchaguzi kwa kura chache, jambo linalompa Bongo fura ya kuongoza taifa hilo kwa muhula mwingine wa miaka saba.
"Walishambulia mwendo wa saa 01:00 (00:00 GMT). Ni kikosi cha wanajeshi walinzi wa rais. Walikuwa wanarusha mabomu kutoka kwa helikopta na kisha baadaye wakashambulia kutoka ardhini," Bw Ping, ambaye hakuwa katika makao makuu hayo wakati huo, alisema awali.
Ameomba usaidizi kutoka kwa jamii ya kimataifa kulinda raia.
Matokeo ya uchaguzi yalitangazwa Jumatano alasiri na kumpatia Bw Bongo ushindi kwa 49.8% ya kura, akifuatwa na Bw Ping aliyepata 48.2 % ya kura, kura zilizowatenganisha zikiwa 5,594.
Bw Ping alisema uchaguzi huo ulijaa udanganyifu na "hakuna ajuaye" hasa nani alishinda.
Waandamanaji waliingia barabarani muda mfupi baada ya tangazo kutolewa. Walichoma moto majengo ya bunge na kukabiliana na polisi wa kuzima fujo.
Upande wa Bw Ping unasema takwimu kutoka ngome za rais huyo zinaonyesha asilimia 99 ya wapiga kura walijitokeza. Ameomba takwimu za wapiga kura kutoka kila kituo zitolewe wazi.
Bw Bongo aliingia madarakani mwaka wa 2009, baada ya kifo cha babake aliyekuwa ameongoza taifa hilo tangu 1967.
Kabla ya kuingia katika siasa, Ping aliwahi kuhudumu kama mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika.
No comments:
Post a Comment