Sherehe ya ufunguzi
wa kongamano kuu la wajumbe wa chama cha Republican nchini Marekani
imegubikwa na utata baada ya hotuba iliyotolewa na mke wa Donald Trump.
Hotuba
hiyo ya Melania inadaiwa kuwa na maandishi yaliyotolewa kutoka kwenye
hotuba ya mke wa Rais Barack Obama, Michelle, aliyoitoa miaka minane
iliyopita.Mke huyo wa Trump, ambaye ni mzaliwa wa Slovenia, amesema alipata usaidizi mdogo sana wakati wa kuandika hotuba hiyo, ambayo imesisitiza sana maadili ya kifamilia na kujumuishwa kwa watu wa matabaka yote.
Sehemu moja ya hotuba ya Bi Trump alisema: "Wazazi wangu walinifunza umuhimu wa kutia bidii kutafuta unachotaka maishani; kwamba neno lako ndilo linaweka uhusiano na unafaa kutenda unachosema na kutimiza ahadi; kwamba lazima uwaheshimu watu.”
Hotuba ya Bi Obama mwaka 2008 ilisema: "Mimi na Barack tulilelewa na maadili karibu sawa, kwamba unatia bidii kutafuta unachotaka maishani; kwamba neno lako linaweka uhusiano na kwamba unafaa kutenda unachosema utatenda; kwamba lazima uwaheshimu watu, hata kama huwafahamu, na hata kama haukubaliani nao.”
Maafisa wa kampeni wa Bw Trump hawajajibu madai hayo.
Wengi wa waliohutubu katika kongamano hilo linaloendelea mjini Cleveland, Ohio, wameangazia sana kutilia shaka uwezo wa mgombea wa chama cha Democratic Hillary Clinton kuwa rais.
Meeya wa zamani wa New York Rudy Giuliani amewauliza wajumbe: “Nani anaweza kumwamini Bi Clinton amlinde?”
Awali, wajumbe wanaompinga Bw Trump waliandamana na kulalamika baada yao kuzuiwa kuwasilisha pingamizi zao.
CHANZO: BBC
No comments:
Post a Comment