Mkulima wa Mpunga akifurahia sehemu ya kazi yake huko Mkoani Ruvuma hivi karibuni
Na, Fulgence Makayula
Kilimo ni uti mgongo wa taifa la Tanzania ambapo
takribani asilimia 60 ya watanzania wote uishi kwa kutegemea kilimo ambacho
kimekuwa mkombozi mkubwa wa maisha yao.
Huku kukiwa na mgawanyiko mkubwa wa maeneo na mazao
ya kilimo maeneo ya kanda ya kaziskazini kilimo cha mazao ya biashara kama vile
kahawa kililimwa kwa wingi pamoja na mazao ya chakula kama vile mahindi,
matunda na viungo kama nyanya, vitunguu, tangawizi na vinginevyo vingi
vikilimwa huko.
Kwa kanda ya ziwa kilimo cha mazao ya biashara
ikiwemo pamba na kahawa kwa mkoa wa Kagera, mazao ya chakula kama mtama,
mahindi, viazi vitamu, uwele na mihogo ndiyo mazao makuu ya chakula yalimwayo
kwenye mikoa hiyo ya kanda ya ziwa.
Lakini kwa kanda nyingine pia mahindi hulimwa kwa
wingi, Alzeti kwa mikoa ya Singida na Manyara kwa kiasi fulani, Morogoro pia
hulimwa mpunga kwa wingi kama ilivyo kwa mikoa ya kanda ya Juu kusini hususani
mkoa wa Mbeya.
Kwa takwimu zilizotolewa kutokana na Sensa ya Watu
na Makazi iliyofanyika mwaka 2012, inaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 65 ya
watanzania wote hutegemea kilimo ili kuendesha maisha yao bila kujali ni kilimo
cha aina gani. Huku wazalishaji wakubwa wakiwa ni wakina mama ambao ushughulika
na shughuli za kilimo ili kukomboa familia na bara zima la njaa na umaskini.
Lakini cha kushangaza hapa vijana ambao wapo zaidi
ya asilimia 54 ya watanzania wote huku wakiwa na nguvu za kutosha kutumika na
kujenga nchi hii kwa kutumia rasilimali zilizopo nchini hususani Ardhi. Wengi
wao wamekuwa wakikimbilia mijini na kuwaacha wazazi wao wakiwatafutia mahitaji
na kuwategemea kwa asilimia kubwa.
Kundi kubwa la wanaoenda mijini hujiusisha na
shughuli za kiuharifu ikiwemo uvutaji wa bangi, ukabaji na uporaji na majanga
mengi ikiwemo lile la kujiuza kwa baadhi ya dada na wakaka ambao ujulikana kwa
majina maarufu ya machangudoa na makakapoa.
jambo hili limekuwa tofauti kwa kijana Kelvin Chombo
ambaye ni mwanafunzi wa chuo kikuu kishiriki cha Elimu Dar Es Salaam ( DUCE),
ambaye ameitumia vizuri fursa ya kilimo
kwa kuanza kulima kilimo cha mpunga. Ambacho yeye mwenyewe anaamini ndicho
kilimo kitakachomkomboa na kumfanya awe na maisha mazuri ya mbeleni.
Na si kubaki
kuishi maisha tegemezi kama vijana wengine waishivyo kwa kubweteka na kusahau
kujishughulisha na shughuli za kilimo kwa kuogopa kuchekwa au kuonwa wa zamani
maana wapo baadhi wana dhana potofu kuwa mtu aliyesoma si sahihi kujiusisha na
masuala ya kilimo.
Kelvin alianza kujishughulisha na kilimo cha mpunga
tangu mwaka 2009, akiwa kidato cha pili huko Mkoani Morogoro,ambapo tangu
kipindi hicho amekuwa akipata mafanikio makubwa ambayo yanamwezesha kuishi
maisha ambayo yeye anaamini kwa kiasi kikubwa ni ya kujitegemea kwa takribani
Asilimia 70.
‘‘Nilianza kulima mpunga tangu nikiwa kidato cha
pili mwaka 2009, ambapo nilikuwa nalima ekari moja ili kujipatia mahitaji yangu
ya shule na chakula cha pale nyumbani. Lakini hii ilichangiwa na wazazi wangu kuwa wakulima hivyo tulishirikiana
kulima mazao mbalimbali kama choroko, migomba, mahindi na mazao mengine ya
chakula yakiwemo maharage. Lakini zao kubwa lilikuwa mpunga ambalo kwa kiasi
kikubwa tulilitegemea na huchangia kupata mahitaji mengi ya shule ikiwemo ada
na baadhi ya mahitaji ya shule hii baada ya kuuza mpunga msimu wa mavuno”
Kelvin anasema, “ hauwezi kuamini nipo hapa chuo
lakini bado najihusisha na kilimo ambako kwa sasa nina ekari tano, ninazomiliki
mwenyewe, huwa nazilima kipindi cha likizo. Na ninapokuwa chuo wazazi wangu
hunisaidia uangalizi wa mashamba yangu, kwa mfano likizo hii iliyoisha majuzi
ya muhula wa kwanza. Ambapo tulifunga chuo kwa muda wa wiki tatu nilienda
kufanya palizi ya shamba langu na kuweka mbolea pamoja na dawa kuuwa magugu”
“Kiukweli nimefanikiwa sana kupitia kilimo na ndicho
kinaniwezesha kujilipia ada yangu hapa chuoni, maana Serikali inanipatia fedha
za kujikimu, chakula na malazi ila ada
najilipia mwenyewe, pia nasaidia familia yangu pamoja na wadogo zangu na huwa
siwasumbui wazazi wangu suala la ada wala matumizi labda niwe naumwa au
kuishiwa kabisa ambap[o huwa ni kwa nadra sana kutokea”
Akiwa ni mzaliwa na mkazi wa Mtimbira mkoani
Morogoro, amekuwa taa na mwangaza kwa
vijana wengine ambao huenda wameshindwa kuchukua hatua za
kujishughulisha na kilimo. Hivyo wanaweza kuona
fursa hii ambayo itawakwamua kimaisha.
Mbali na hayo Kelvin anaendelea kuwaasa vijana
wenzake kuwa , “kilimo ni kizuri mno maana ni ajira isiyo tumia gharama kubwa na
mtu unaweza usiwe na mtaji wowote zaidi
ya mbegu, mtaji ni nguvu zako. Hii ni shughuli ambayo inamuingizia mtu kipato
pasipo kuwa na gharama kubwa ya kianzio.
Maana vijana
wengi wanashindwa kujitoa wakidai hawana mtaji, lakini kwenye kilimo hakuna
kusema kwamba unahitaji mtaji mkubwa kiasi gani, kama mwenyewe pia unajishughulisha
basi utajikwamua katika hali ya utegemezi na hatimaye msimu ukifika unapata
kianzio chako. Sasa kama unataka kutoka
kwa mtaji basi hapo sasa kilimo kinakupatia mtaji.”
Na kuongeza kwa shairi moja maarufu ambalo linaitwa
kama unataka mali utaipata shambani, maana hakuna mbadala wa shamba maana
waswahili usema mtaji wa maskini ni nguvu zake mwenyewe.
Na anatumia mwanya huu kuwasihi vijana wenzake
kuepukana na mawazo mgando, na badala yake waone kilimo kama ni fursa pekee
ambayo pia inaweza kuwatafutia mtaji wa kujiajiri wenyewe.
John Nyaluchi, ni rafiki mkubwa wa Kelvin ambaye wanasoma naye chuoni hapo yeye anasema
“ nimemfahamu Kelvin kwa muda mrefu sasa, na amekuwa fundisho kubwa kwenye
maisha yangu , jinsi anavyojishughulisha na shughuli za kilimo. Kwani nilipata
fursa ya kwenda Morogoro kuona kama anachoniambia ni kweli, kwa kweli amekuwa
fundisho kubwa si kwangu tu hata kwa vijana wengine hapa chuoni na nje pia.
Mzee Chombo ni baba mzazi wa Kelvin anasema “ nina muamini
sana kijana wangu kwa kuwa tangu amejikita kwenye kilimo cha mpunga ametusaidia
sana hapa nyumbani, hata wadogo zake maana muda mwingine nikikosa kabisa fedha
ya kuwapeleka wadogo zake shule, nampigia simu anasema tuuze mpunga wake, na
tunafanya hivyo”
Hivyo basi vijana wa kitanzania ni vyema kuona fursa
zilizo kwenye maeneo yao kwa kutumia rasirimali zilizopo nchini ikiwemo ardhi
ambayo imejaa rotuba kwa kilimo cha mazao mbalimbali yakiwemo ya chakula,
mbogamboga, matunda pamoja na mazao ya biashara ambayo yatainua kipato cha
mmoja mmoja.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika na watu
wake pia wakiwemo vijana wenye nguvu za kufanya kazi za uzalishaji mali. Ili
kupunguza vitendo vya ubakaji, uporaji, uvutaji madawa ya kulevya, na kukaa vijiweni
pasipo kujishughulisha.
No comments:
Post a Comment