Waziri wa Elimu, sayansi, teknolojia na mafunzo ya ufundi, Dr. Joyce Ndarichako
Na, BARAKA NGOFIRA
0763580901, 0716216249
Ni ukweli usiofichika kuwa elimu yetu
ilikuwa imepoteza dira na mwelekeo, watu wengi walikuwa wameka tamaa na namna
mfumo wa elimu yetu ulivyokuwa unaendeshwa na baadhi ya watendaji wengi
waliopita kwenye wizara hii pasipo kujali
unyeti wake. Kwa kusahau kuwa pasipo msingi wa elimu bora ni sawa na
utumwa na ujinga ambao uasababisha baadhi ya watu kushindwa kujua wapi watokapo
na wapi waendapo.
Kwanza nikupongeze sana maana nilitamani
sana siku moja uje uwe mkuu kwenye wizara hii nyeti ambayo ni kiwanda na injini
ya nchi ya kuzalisha na kupika wasomi na wataalam katika fani mbalimbali. Hii
pia ilikuwa ni hamu kubwa wa wanaopenda maendeleo ya sekta ya elimu hapa
nchini.
Pia, Nimpongeze Rais Dk. Magufuli kwa
kukuona na kukuchagua uwe jembe letu kwenye wizara hii nyeti ya elimu, naamini
wewe ni jembe na hilo hakuna anayebisha, na kama yupo basi atakuwa na matatizo
yake binafsi katika lile ulilokuwa unalisimamia kabla haujapewa wadhifa huu
mkubwa wa kutekeleza kauli mbiu ya hapa kazi tu, ambayo naamini ni kazi
kwelikweli.
Nafahamu ni wizara kubwa kwako lakini
naamini unaweza kwani wadau wa elimu tunakuombea ili upambane vilivyo ili
uwashinde wale wanaotaka elimu yetu isiwe na thamani, wasomi wengi kuzurura
mitaani na vyeti vyao huku wakitafuta ajira pasipo mafanikio. Na kubezwa na
waajiri kuwa hawana sifa na hawajui
lolote na vyeti wamegawiwa tu. Naamini litapungua au kuisha kabisa.
Nakumbuka utendaji kazi wako uliotukuka
ulipokuwa Baraza la Mitihani, umeandika historia kama kiongozi shupavu tena
mwanamama ambapo kila apendaye maendeleo ya elimu atosita kukuita jasiri, kwa
hili unastahili pongezi nyingi za dhati kwa kutokubali kuyumbishwa na
wasioitakia mema nchi yetu, na kusimama na msimamo wako kwa kusimamia kile
ulichokiamini kinajenga na kuimairisha elimu yetu.
Na sasa umekuwa waziri baada ya
kuteuliwa na Dr. Magufuli, kwa niaba ya wengine wote niseme karibu sana kwenye
wizara ya elimu. Lakini ni imani yangu kuwa unayajua mapungufu yaliyopo kwenye
wizara uliyokabithiwa. Mapungufu na matatizo yamekuwa ni ya muda mrefu ambayo
mengine kwa kiasi fulani yamesababishwa na viongozi wetu lakini mengine ni
masuala tu ya muda na fedha ndio chanzo kikubwa cha matatizo hayo.
Mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu
ambayo imekuwa ikitolewa kiubaguzi kwa kuzingatia fani na masomo wasomayo
wanafunzi imekuwa ni tatizo kubwa ambalo limesabibisha vijana wengi kukimbilia
ualimu. Jambo ambalo limesababisha kuwa na idadi kubwa ya walimu ambao
wamewageuza wanafunzi vitega uchumi vyao kwa kuwaongezea michango mingi na
isiyo na maana, ni kwa sababu ndoto zao hazikuwa kuwa waalimu bali kitu kingine
tofauti, lakini kwa sababu tu ya kuogopa kusota mtaani pila kusoma au kulima
kwa sabababu ya kukosa mkopo ndiyo maana wameamua kukimbilia huko kwenye
ualimu.
Siku
hizi ualimu umekuwa dili la haraka na ambalo wanajifariji kuwa halikosi mteja
maana shule ni nyingi na wanafunzi kila mwaka wanaongezeka. Hiyo ni hoja lakini
jiulize kila mwaka wanaajiliwa waalimu wangapi kwenda kufundisha wanafunzi
hawa?
Je
ufaulu umeongezeka au umepungua ukiringanisha na miaka kumi ya nyuma? Msomaji
wangu ukisha jiuliza maswali hayo njoo uwaone waalimu hawa nyumba waishizo je
zina hadhi ya wao kuishi? Nyingine zimejazana vichuguu na mchwa ambao wameamua
kuishi ili wakiacha karatasi za wanafunzi wawasaidie kutunza.
Jiulize
tena ni dada zetu wangapi walikuwa wanashindwa kumaliza masomo yao ya msingi
ama sekondari kwa sababu ya kupata ujauzito kwa miaka kumi au 20 iliyopita na
ukiringanisha na leo ni wanafunzi wangapi wameshindwa kuhitimu masomo yao kwa
sababu ya mimba walizopewa na walimu wao? Jibu unalo mwenyewe msomaji.
Sijui
nielezeje, lakini kwa kifupi ni kuwa imewabidi wawe waalimu wasio na nidhamu na
kuondokewa na hofu ya kazi kwa sababu tu iliwalazimu wakasomee ualimu kwa
sababu ni kipaumbele cha wao kupata mkopo na ajira kwa urahisi. Ukiringanishwa
na fani nyingine ambazo wengine wanazisoma.
Waswahili
wanasema utavuna ulichopanda, na ndicho sasa tunakivuna kwenye elimu yetu
kuanzia msingi hadi vyuo vikuu, ni aibu tena aibu ambayo tena ni aibu hata
kuiongelea. Serikali ilianzisha mikakati mingi tu ili kuwafanya watu wengi
wapende kusoma ualimu lakini kwa hili la kuwabagua wanafunzi kwenye mikopo
iliharibu kabisa.
Japo
kwa kiasi kikubwa imefanikiwa kuwapata walimu wengi lakini walimu wasio na
ualimu na maadili ya kazi, waliojika mavazi ya ualimu lakini roho zao wakiwa
wajasiriamali wakubwa kwa kugeuza bidhaa ambazo ni michango isiyo na kichwa
wala miguu kwa wanafunzi wawafundishao.
Utasikia
mtoto wa darasa la kwanza akimuomba mzazi wake pesa kwa ajili ya masomo ya
ziada ambayo hata mzazi mwenyewe unachanganyikiwa, na kujiuliza maswali kuwa
huyu mtoto anasoma masomo yapi ya ziada ambayo tena ni lazima awapelekee walimu
walewale wanaomfundisha? Ndo jibu unalipata kuwa ni miradi au wanafunzi
wamegeuzwa vitega uchumi vya walimu.
Nina
imani Dr. Ndarichako uozo kwenye elimu kamwe hautoufumbia macho kabisa,
tunaitaji elimu yetu iimarike ili ituwezeshe kurimudu vyema soko la ajira kama
vijana wa nchi nyingine zinazonguka wanavyotushinda sokoni. Kwako watanzania
wana imani kubwa kuwa hautotuangusha maana wewe ni jembe haushindwi kitu,
tunakuombea uweze kutumbua majipu na wale wajifanyao miungu watu huku
wakivuruga na kutuharibia elimu yetu.
Zaidi
ya yote Mungu akulinde na kukuongoza ili uwe na akili fikra na uwezo mkubwa wa
kupambana na matatizo yaliopo kwenye wizara hii nyeti na muhimu kwenye ukuaji
wa taifa letu. Hapa ni kazi tu na iwe kazi kweli kweli.
Mungu Ibariki Tanzania, Mungu ibariki wizara
ya elimu, sayansi na maendeleo ya jamii ili iweze kuwa mwangaza na taa ya
wataanzania kututoa kwenye wimbi la umaskini, magonjwa na ujinga. Pia mbariki
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. magufuli na watendaji wake katika kutuletea
mabaadiliko ya kweli nchini kwetu.
Makala
haya yameandikwa na Baraka Ngofira, mwanafunzi wa Mawasiliano kwa Umma (mwaka
wa pili) katika shule kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma ya Chuo
Kikuu cha Dar es salaam (UDSM-SJMC). Anapatikana kwa mawasiliano ya 0763580901,
0716216249 au e mail ya
barakangofira@gmail.com.
No comments:
Post a Comment